USIMKUBALI KILA MTU,NA USIMKATAE KILA MTU:

| Makala

USIMKUBALI KILA MTU,NA USIMKATAE KILA MTU:

Maisha ni siri kubwa sana ambayo hiyo siri ipo mikononi mwa Mungu mwenyewe aliyetuumba na kutuweka hapa duniani.

Sijui kama unajua ila kama unajua basi nataka nikujuze zaidi kidogo hapa siku ya leo.

Baraka na laana zipo ndani ya mtu unayemuona mbele yako,au huyo unayeishi nae sasahivi.

Labda nirahisishe mazungumzo yangu ili unielewe vizuri zaidi,maana lengo langu ni kukupa maarifa yatakayokusaidia kwenye maisha yako.

Mungu anapotaka kukubariki na kukuinua kwenye maisha yako, huwa anakuletea mtu au watu sahihi maishani mwako.

Hivyo hivyo na shetani pia, yeye akitaka kuyaharibu maisha yako na kukuvuruga kabisa huwa anakuletea mtu au watu wasio sahihi kwako.

Tufuatane kwa maandiko kabisa ya biblia.utanielewa zaidi hapa….Isaya 43:4 

Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.

Hii ni kauli ya Mungu mwenyewe, anasema atainua watu na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako wewe unayesoma ujumbe huu…..

Unakumbuka kitu kilichomuangusha samsoni mpaka akakamatwa na maadui zake??? Nakuachia swali utalijibu kwa wakati wako.

Maelezo ni mengi sana kwenye biblia na hatuna muda wa kutosha kuandika kila kitu hapa, lakini kile ninachotaka ukione na ukielewe ni kwamba, mtu anaweza kutumiwa na Mungu kukubariki, na pia mtu huyohuyo anaweza kutumiwa na shetani kuyaharibu maisha yako kabisa.

Kuna watu ni mashahidi wa hiki ninachokisema hapa, wapo watu na huenda ni wewe kabisa unayesoma ujumbe huu, maisha yako yameshuka gafla na kuvurugika kabisa baada tu ya kumfungulia mtu mlango wa maisha yako, na pia kuna mwingine maisha yake yameanza kupanda na kupata thamani pale alipomfungulia mtu fulani mlango wa maisha yake.

narudia kusema kuwa sio kila mtu unapaswa kumfungulia mlango wa maisha yako, na sio kila mtu unapaswa kumfungia mlango wa maisha yako.

Wala sikuchanganyi kabisa, unajua cha kufanya mtu wa Mungu.

Yesu kabla ya kuchagua wanafunzi wake 12 wa kushirikiana nao kwenye huduma yake, alipanda mlimani usiku kwa ajili ya kuomba, aliomba usiku kucha, sawa na masaa 12 ya kuwaombea wanafunzi 12, maana yake kila mwanafunzi wa Yesu aliombewa lisaa lizima kabla ya kuchaguliwa kuingia kwenye huduma.

Nikuulize swali dogo mtu wa Mungu, hao watu unaotaka kushirikiana nao kwenye biashara yako au kazi yako,umewaombea? Na kama umewaombea Mungu amekuonyesha nini kuhusu wao? Amekuruhusu uendelee nao au uachane nao?

Na huyo mchumba unayetaka kuingia nae kwenye ndoa je, uliomba? Au utaomba mkishaingia kwenye ndoa?

Kujengwa na kuharibiwa kwa maisha yetu,tunasababisha wenyewe na maamuzi tunayoyachukua kila siku.

Nakupenda na ndio maana nakushirikisha mambo haya kwa faida yako na maisha yako.

Ukihitaji maombi na maombezi,ushauri wa kiroho pia na mafundisho ya neno la Mungu, nitumie ujumbe mfupi wa majina yako kwa Whatssap kupitia namba +255 758 708804 popote ulipo, nitakuunga kwenye group la maombi ya kila siku usiku.

Pastor Innocent Mashauri

Madhabahu ya SIRI ZA BIBLIA

Maarifa ya ki-Mungu


 SADAKA